Kisii na Maseno Zang'aa katika KUSA Western Conference ya Mpira wa Mikono

Kisii na Maseno Zang'aa katika KUSA Western Conference ya Mpira wa Mikono
Chuo kikuu cha Maseno na Kisii, Picha Mwana wa Africa

Na Mwana wa Africa 

Chuo cha Kisii na Maseno vimeonesha uwezo mkubwa katika mashindano ya kufuzu nusu fainali katika michezo ya Mpira wa Mikono yaliyoandaliwa katika Chuo Kikuu cha Kisii Jumamosi tarehe 16 Machi.

Kisii walionyesha utendaji wao bora katika Kundi A, ambapo walishinda kwa alama 23-22 dhidi ya Jaramogi na 42-22 dhidi ya Great Lakes University of Kisumu. Hivyo, Kisii wamefuzu nusu fainali ambapo watakutana na Kaimosi.

Jaramogi, ingawa walionyesha mchezo mzuri katika kipindi cha kwanza, walishindwa katika kipindi cha pili na hatimaye kupata kichapo. Hata hivyo, walijirekebisha na kushinda katika mechi ya pili dhidi ya Great Lakes University of Kisumu kwa alama 49-19, na hivyo kufuzu nusu fainali ambapo watakutana na Chuo cha Maseno.

Katika Kundi A, Chuo cha Kisii kiliongoza kwa alama 6, wakiwa na alama tatu mbele ya Jaramogi walio na alama 3. Great Lakes wamebanduliwa katika mashindano hayo kwa kumaliza wa tatu, sawia na Chuo cha Kabianga ambacho kilimaliza bila alama yeyote katika Kundi B.

Katika Kundi B, Maseno waliibuka kinara kwa alama 6, wakiwa na alama tatu mbele ya Kaimosi waliofuzu kwa alama 3.

Maseno waliwashinda Kaimosi katika mechi ya kwanza ya Kundi B kwa alama 34-27 na 28-22 dhidi ya Kabianga. Kaimosi walifuzu kwa kuwashinda Kabianga 24-21.

Katika ratiba ya nusu fainali itakayochezwa Jumapili, Kisii watapambana na Kaimosi wakati Maseno watakutana na Jaramogi. Washindi wa mechi hizo mbili watakutana katika fainali itakayofuata baada ya nusu fainali.

Timu za kwanza na pili zitashiriki katika michezo ya Kitaifa itakayoandaliwa na Chuo Kikuu cha Masinde Muliro tarehe 29 Machi 2024.