Mwanariadha Charles Kipsang Aaga Dunia Katika Mbio za Mount Cameroon Race

Charles Kipsang alianguka na kufariki huko Cameroon katika mashindano ya 29 ya Mount Cameroon Race of Hope siku ya Jumamosi, tarehe 24 Februari 2024.

Mwanariadha Charles Kipsang Aaga Dunia Katika Mbio za Mount Cameroon Race
Mwanariadha Charles Kipsang

Na Mwana wa Afrika 

Kenya imempoteza mwanariadha mwingine wiki mbili baada ya kifo cha mshikilizi wa rekodi ya dunia Kiptum.

Kiptum aliyeaga kutokana na ajali ya barabara pamoja na kocha wake Hakizimana katika barabara ya kuelekea Eldoret karibu na msitu wa Kaptagat.

Charles Kipsang alianguka na kufariki huko Cameroon katika mashindano ya 29 ya Mount Cameroon Race of Hope siku ya Jumamosi, tarehe 24 Februari 2024.

Licha ya mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 32 kuongoza mbio hizo, alionekana kushindwa na safari katika mtari wa mwisho ili kutawazwa mshindi, jambo ambalo lilipelekea yeye kumaliza nafasi ya 16.

Kipsang, ambaye alikuwa mwanariadha wa kwanza wa Kenya kushiriki katika mbio hizo, alianza mwaka wake akiwa katika fomu nzuri.

Aliaga dunia wakati madaktari walipokuwa wakijaribu kumpa huduma ya kwanza katika uwanja wa Molyko huko Cameroon.

Aidha, Gavana Bernard Okalia alithibitisha kifo cha Kipsang katika hospitali ya Buea Regional Hospital Jumamosi jioni, huku chanzo cha kifo chake kikibakia kuwa kuzungumkuti.

Shirika la Uwanahabari la Cameroon limesema kwamba madaktari wa Buea Regional Hospital walitoa taarifa baada ya kufanya utafiti na kusema kuwa huenda mshtuko wa moyo ulikuwa chanzo cha kifo chake.