Lazio 1-0 Bayern Munich: Je, Tuchel atapigwa kalamu?
Na Mwana Wa Afrika
Vigogo wa Bundesliga Bayern Munich walikubali kichapo cha 1-0 usiku wa jana katika uwanja wa nyumbani wa Lazio Olimpico katika mashindano ya mwondoano wa raundi 16 ya Klabu Bingwa Ulaya.
Bayern Munich imezidi kuonyesha matokeo mabovu katika mechi mbili zilizopita chini ya mkufunzi Thomas Tuchel. Hii ni mechi ya pili kukamilika bila ya vijana hao wa Tuchel kupata ushindi wowote.
Baada ya kichapo cha 3-0 jumamosi na Bayern Liverkusen, usiku wa jana, vijana wa Tuchel walilazimika kupokea adhabu ya Lazio kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Immobile dakika ya 69 baada ya beki D. Upamecano kumchezea vibaya Gustav Isaksen ndani ya sanduku. Upamecano, alipewa kadi nyekundu dakika ya 67 na huenda akakosa mechi ya marudiano tarehe 5 Machi.
Bayern Munich walifeli kulenga shabaha ndani ya goli la Lazio dakika tisini. Kupitia kichapo hicho, Tuchel yumo na wasisi wa kupigwa kalamu wakati wowote.
Akizungumza na TNT Sports Tuchel alisema kuwa,"Tumehuzunika na tuko na hasira baada ya kupata kichapo. Inaonekana wazi tulishindwa katika mechi, na inawezekana Lazio walitushinda. Nilijaribu kuwahamasisha vijana wangu kurejesha nguvu katika kipindi cha pili, lakini bahati haikuwa upande wetu. Tulipoteza nafasi nyingi katika kipindi cha kwanza. Natumai kwamba tutaweza kujirekebisha nyumbani katika mkondo wa pili."
Bayern Munich watawaalika Lazio nyumbani Allianz Arena katika mechi ya marudiano. Bayern watalazimika kufunga mabao 2 -0, 3-0 au zaidi ili kuweza kutinga katika robo fainali.
Matokeo mengine ya usiku wa jana ya Klabu Bingwa BaraniUlaya: PSG 2-0 Real Sociedad.
Mechi za Leo UEFA Europa: Feyenoord Vs Roma, Galatasaray Vs Sparta Prague, S. Donetsk Vs Marseille, AC Millan Vs Rennes, Benfica Vs Toulouse, Braga Vs Qarabag FK, Lens Vs Freiburg.